ID 2E48C4
Habari, mimi na msichana wa miaka 20, sijui nianzie wapi, naumia sana sana, lakini naamini kwenu naweza pata faraja. Natokea mkoa wa kagera na nilikuja Dar kufanya kazi za ndani, nipo maeneo ya mbagala kwa sasa ambapo ndo ninapofanyia kazi.
Nilishindwa kuendelea na masomo na niliishia form two kwa ajili ya ugumu wa maisha nyumbani. Nilikua na ndoto nyingi, niliamini kua mimi ndo nitaikomboa familia yangu yani wazazi wangu. Hata pale nilishindwa kuendelea na masomo bado nilijipa imani ya kutokukata tamaa.
Nilitamani sana kuja mjini kufanya kazi, ndipo mama yangu alinifanyia mpango, na nikaweza kuja mjini Dar, ambapo ndo huku ninapofanyia kazi hadi sasa. Nikajua huu ndio mwanzo mzuri wa safari ya maisha yangu.
Ni kweli ndoto yangu ya kuja mjini ilitimia lakini sivyo nilivyotegemea, ni miezi kadhaa tu tangu nije hapa nilipo lakini imekua kama miaka kumi, nateseka sana, yani huyu mama ambaye ndiye boss wangu pamoja na mumewe wananipa maumivu sana jamani.
Mambo ni mengi sana humu ndani, naishi mimi na hawa maboss zangu pamoja na watoto wao wawili wakubwa, na wengine wapo shuleni, ila hawa wakubwa wanafanya kazi hivyo mara nyingi hua nipo mwenyewe nyumbani.
Muonekano wa nyumba ni kubwa na ina geti vizuri, unaweza sema hamna shida yoyote humo ndani lakini sivyo. Wakiondoka asubuhi naambiwa nichemshe mihogo mingi nitakayoweza kula asubuhi, mchana kila siku iendayo kwa mungu, yani hicho ndicho chakula changu.
Wageni wakija ndo hua nafuu yangu. nafokewa muda wote na huyu boss wangu wa kike. ananipa hadi chupi zake zenye uchafu wa kipindi cha mwezi nizifue. Kinachoniuma zaidi ni huyu mwanae wa kiume mkubwa, hua ananyata usiku anaingia chumbani kwangu kwakua mlango wangu haufungi vizuri, kitasa chake kimeharibika.
Mwanzoni nilimuona na alikimbia, nikajaribu kumwambia huyu mama anirekebishie kitasa cha mlango lakini alinijibu kua hakuna wa kunifatilia huko chumbani. nilikaa kimya, juzi juzi hapa aliingia chumbani kwangu na kutaka kunibaka, mimi nina mwili mdogo na yeye ana mwili mkubwa.
Alitumia nguvu nyingi sana na nilijitahidi nisipige kelele, na alikua kanikaba na kunikwaruza sehemu zingine za mwili wangu, nilijitahidi niwezavyo asifanikiwe, na alivyoona hivyo akakimbia na kutoka chumbani, nililia sana usiku ule na nikaenda kumgongea mama -boss, nikamwambie kilichokua kinaendelea.
Huwezi amini yule mama alinikatalia katakata kua mwanae hawezi kufanya kitu kama hicho. nilivunjika moyo sana kwakua sikua na mtetezi, mara nyingi nilikua naongea na baba yangu mzazi na nikamwambia nataka kurudi nyumbani kazi imenishinda, lakini alinisisitiza nivumilie kidogo.
Sikua namwambia yote yanayotokea ya kutaka kubakwa na manyanyaso, hivyo yeye alinisisitiza nipambane na kazi. nilitamani kumshtakia na hili tukio lakini hivi karibuni simpati kwenye simu na mama nae simu hana. kiukweli nataka kurudi nyumbani, na kingine kwa muda wote niliokaa sijawahi kulipwa zaidi ya mwezi mmoja tu.
Ni ule mwezi wa kwanza nilioanza kazi, na nilimwambia boss wangu amtumie baba yangu hiyo pesa, na hii simu niliyonayo alininunulia boss wangu wa kiume kwasababau ya mawasiliano ya hapa nyumbani wakiwa hawapo.
Comments
No comments yet. Be the first to share a thought.