ID EBD1D0
Miaka mitano iliyopita, maisha yangu yalibadilika ghafla. Mwanangu aliyekuwa kijana alikuwa ameficha jambo kwa hofu kubwa—alimpa msichana mimba. Msichana huyo alitoka kwenye familia tajiri sana, na hatukujua kabisa kuhusu ujauzito huo hadi baada ya mtoto kuzaliwa.
Asubuhi moja, kulikuwa na kelele nje ya nyumba yetu. Nilipotoka kwa haraka, nilimkuta mwanangu analia, akiomba msamaha. Wazazi wa msichana walikuwa pale, wakiwa na hasira kali. Walizunguka nyumba yetu na wakaweka wazi kuwa walituona hatufai kwa binti yao. Walisema binti yao alikuwa bado mdogo sana kuwa mama, na hastahili kufungamanishwa na familia ambayo wao waliamini ni masikini.
Wakati huo, mwanangu alikuwa anasoma shule ya kutwa ya kawaida, wakati binti yao alikuwa anasoma shule maarufu ya bweni. Kwao, tofauti ya maisha yetu ilimaanisha hatuko sawa.
Baada ya binti kujifungua, walikuja na mtoto, akiwa na siku moja tu tangu azaliwe, amefungwa kwa kitambaa kidogo. Moyo wangu ulivunjika nilipomwangalia yule mtoto asiye na hatia. Niliwaomba wamuache msichana akae nasi hata miezi michache ili amnyonyeshe mtoto wake. Niliwaahidi nitamlea mama na mtoto kwa upendo na uangalizi wote. Lakini walikataa kabisa. Walisema binti yao hatatunzwa vizuri kama angekaa kwetu.
Kabla ya kuondoka, walichukua hata kile kitambaa alichofungwa mtoto, wakisema hawataki chochote chao kibaki kwetu. Walituachia mtoto na wakaondoka. Siku hiyo, sikua tena bibi tu—nilirudi kuwa mama. Nilimlea mtoto kupitia usiku wa kukosa usingizi na nyakati ngumu sana.
Leo, mjukuu ametimiza zaidi ya miaka saba, tena ni mwenye afya njema na furaha tele. Ananiita 'Mama' kwa sababu mimi ndiye mama pekee aliyewahi kumjua.
Hivi karibuni, familia ya msichana imerudi. Binti yao sasa ameolewa, lakini ameshindwa kupata watoto. Sasa wanataka mtoto arudishwe ili mama yake mzazi aweze 'kuzoeana' naye.
Moyo wangu umevunjika vipande viwili. Nitawezaje kuachia mtoto niliyemlea kwa upendo na kujitoa mhanga?, Kwake, mimi ndiye nyumbani. Mimi ndiye mama yake. Kipindi kile walimwacha alipowahitaji zaidi. Sasa hali yao imebadilika, wanataka kumchukua tena. kwakweli sitokuja kuruhusu hilo jambo na niliwakatalia katakata, nipo radhi hata tufikishane mahakamani kwa uwezo wangu huu huu wa kawaida, haijalishi hata kama wao wanafedha.
Comments
No comments yet. Be the first to share a thought.